Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan ametangaza nia yake ya kutaka kujiuzulu kuruhusu uchaguzi mpya wa mapema wa bunge ufanyike.
Pashinyan ametangaza uamuzi wake huo leo wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Armavir ambapo amesema atajiuzulu mwezi Aprili.
Atabakia katika nafasi hiyo mpaka uchaguzi utakapofanyika. Uchaguzi umepangwa kufanyika Juni 20, mwaka huu na ndio hatua pekee itakayoiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa.
Tangu vilipomalizika vita katika jimbo la Nagorno Karabakh, Waziri Mkuu Pashinyan amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa baada ya ardhi kubwa ya Armenia kukabidhiwa Azerbaijan.