Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2019 kutokana na kazi aliyoifanya kumaliza taharuki ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Eritrea.
Abiy alifanikiwa kukamilisha makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili yaliyomaliza vita na taharuki ya kijeshi iliyokuwepo kwa takribani miaka 20. Taharuki hiyo ilitokana na vita ya kugombea mpaka kati ya mwaka 1998 na mwaka 2000.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya 100 ya Nobel, mwanasiasa huyo anatarajiwa kukabidhiwa rasmi tuzo hiyo Disemba mwaka huu.
Aidha, tuzo hiyo itaambatana na kitita cha $900,000 ambazo ni sawa na Sh 20.7 bilioni za Tanzania.
“Nashukuru sana. Ni tuzo ambayo Afrika imepewa, Ethiopia imepewa na ninapata taswira ni kwa kiasi gani viongozi wengine wa Afrika wataichukulia kwa mtazamo chanya katika kuhakikisha amani inadumu kwenye bara letu,” alisema Waziri Mkuu Abiy alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Kamati ya Tuzo ya Nobel.
Abiy amekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia tangu mwaka 2018. Tangu aliposhika nafasi hiyo alitangaza kampeni ya kuhakikisha nchi inarejea katika hali ya amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kuvunja makundi hasimu.
Jumla ya washiriki 301 waliwania tuzo hiyo ambapo kati yao watu binafsi walikuwa 223 na taasisi zilikuwa 78.