Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara ya TAMISEMI sio ngumu ila ni kubwa huku akisisitiza kufanya kazi kwa Ushirikiano na nguvu kazi ndani ya Wizara hiyo ili kuweza kutimiza wajibu na kufikia malengo.
Waziri Ummy amesema hayo wakati akishukuru kwa salamu za ukaribisho baada ya kuripoti Ofisi za TAMISEMI kwa mara ya kwanza, kama Waziri wa Wizara hiyo baada ya kula kiapo Ikulu, jijini Dodoma.
“Kuna watu wanasema TAMISEMI ni ngumu, kwangu mimi TAMISEMI sio ngumu, kama TAMISEMI ni ngumu maana yake mmeshindwa kunisaidia mimi na Manaibu Waziri kutekeleza wajibu wetu, ila tunakubali ni kubwa, lakini hakuna kigumu endapo una ‘team work’ (nguvu kazi),” amesema Waziri Ummy.
Aidha, amebainisha kuwa Waziri aliyetangulia katika Wizara hiyo Selemani Jafo, alifanya kazi nzuri na kubwa kwani Wakati anaingia TAMISEMI mapato yalikuwa asilimia 60 na mpaka anakabidhi Wizara hiyo mapato yalikuwa yamefikia asilimia 94.
Waziri Ummy amesisitiza kuimarishwa kwa usimamizi wa makusanyo ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kusimamia matumizi katika mamlaka hizo ili waweze kutatua changamoto za wananchi.