Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amewahasa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapanga wamachinga bila kutumia mabavu.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa kufungua kikao kazi cha siku mbili na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema uwa ni vyema wakatumia mwezi mmoja uliotolewa kuwaelimisha na kuwashirikisha wamachinga katika kupanga miji.
Septemba 13 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo Kwa halmashauri za Majiji na manispaa kuwapanga wamachinga na Waziri Mkuu alitoa maelekezo ya kutekeleza hilo ndani ya mwezi mmoja.
“Nataka kusisitiza tutumie mwezi mmoja huu kutoa elimu Kwa wamachinga na kuhakikisha wanashirikishwa katika kupanga miji, Tujitahidi sana kutotumia nguvu na mabavu, tutekeleze maagizo ya Rais huku tukizingatia sheria, taratibu na kanuni na kuwashirikisha na kuandaa maeneo ya kuwapeleka,” Amesema Waziri Ummy.
Sambamba na hayo yote Waziri Ummy pia amewataka wakurugenzi hao kuwatengea wafanyabiashara wadogo maeneo ambayo ni rafiki na biashara lakini pia kuwe na mazingira ya wananchi kufikika kufuata mahitaji yao.