Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Magesa Boniphace kupisha uchunguzi.
Taarifa iliyotolewa leo Aprili 20, 2021, Waziri Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo kutoka kwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwemo mbunge wa Sengerema (CCM), Hamisi Tabasamu.
Katika taarifa hiyo, imeelezwa kuwa mkurugenzi na baadhi ya wakuu wa idara za halmashauri hiyo zinaonyesha wanafanya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo.
Pia, amemuelekeza mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha katika kipindi chote ambacho timu ya uchunguzi itakua ikifanya kazi katika halmashauri hiyo malipo yote yatakayofanyika kuanzia sasa yazingatie sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma.
Waziri Ummy amemuagiza katibu mkuu Tamisemi kuunda timu ya uchunguzi wa tuhuma hizo haraka.