Kundi la wezi walioiba Pombe katika Duka vinywaji vikali Nchini Afrika Kusini wameonekana wakilazimishwa kunywa Pombe walizoiba katika video fupi inayosambaa katika mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa baadhi ya Mitandao ya kijamii Nchini humo, tukio hilo lilitokea baada ya wezi, wapatao watatu, kukamatwa na wamiliki wa duka hilo siku chache baada ya kutenda kosa la wizi.
Lakini badala ya kuchukua hatua za vurugu au kuwaita Polisi, wamiliki hao walichukua njia isiyotarajiwa – kuwalazimisha wezi hao kunywa pombe walizoiba hadi dakika ya mwisho.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, wameunga mkono adhabu hiyo wakiona ni njia ya kipekee ya kutoa haki, huku wengine wakielezea wasiwasi wao kuhusu athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na pombe hasa madhara ya figo na hata kupelekea kifo kutokana na unywaji wa kiasi kikubwa cha pombe.
Itakumbukwa mwaka 2020, wakati wa kilele cha janga la Covid-19, kundi la wezi lilichimba handaki chini ya duka maarufu la pombe nchini Afrika Kusini, ambapo walifanikiwa kuvunja sakafu ya zege ili kuiba pombe yenye thamani ya takriban Randi 300,000.