Uongozi wa Simba SC umesema kitendo cha wapinzani wao katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Jwaneng Galaxy cha kubadilisha Uwanja walikishtukia kabla, kwa hiyo hakitawatoa mchezoni.

Simba SC itacheza ugenini nchini Botswana Jumamosi (Desemba 02), baada ya kuanza kwa kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Awali Jwaneng Galaxy wanaoongoza msimamo wa Kundi B, baada ya kucheza mchezo mmoja wa hatua ya Makundi, walipanga kuutumia Uwanja Taifa wa Botswana, lakini sasa wamehamishia mchezo huo kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume uliopo mjini Francistown ambako kuna umbali mrefu kutoka mjini Gaborone.

Mratibu wa Simba SC Abbas Ally amesema tayari walijipanga kukabiliana na changamoto watakazokuna nazo nchini Botswana, lakini suala la mabadiliko ya Uwanja ni la kawaida kwao.

Abbas amesema malengo makuu yanayowapeleka ugenini ni kucheza soka la ushindani ili kupata alama tatu, ambazo zitawaweka katika mazingira mazuri ya kufikia mipango ya kutinga Robo Fainali, na kisha kuendelea na mikakati ya kwenda Nusu Fainali itakapowezekana.

“Suala la kubadilisha uwanja sisi tulishaanza kulipata toka awali hivyo tumejipanga kukabiliana na hilo, ingekuwa mchezo unachezwa nje ya nchi wa Botswana tungesema mengine hivyo hatuwezi kutoka mchezoni kwa sababu ya aina hiyo.”

Simba SC inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi B, kwa kumiliki alama moja sawa na Asec Mimosas inayoshika nafasi ya pili, huku Jwaneng Galaxy ikiongoza kundi hilo kwa kuwa na alama tatu. Wydad Casablanca ya Morocco inaburuza mkia wa Kundi B ikiwa haina alama yoyote, kufuatia kukubali kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy iliyokuwa ugenini.

CPC wakumbuka mchango wa Tanzania kurejeshewa Kiti
Wezi wapewa adhabu ya kunywa Pombe