Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Chakula Duniani World Food Programme (WFP), limetunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2020.
Kamati ya tuzo hiyo nchini Norway imesema kwamba WFP imehusika pakubwa katika juhudi za kuzuia utumiaji wa njaa kama silaha ya vita na mizozo.
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo hiyo mjini Oslo, Berit Reiss Andersen amesema ni vyema dunia kuangaza kuhusu mamilioni ya watu ambao wanakabiliwa na tishio la baa la njaa.
Shirika la Afya Duniani na mwanaharakati wa masuala ya anga Greta Thunberg walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakipigiwa upatu kushinda tuzo hiyo.
Mwaka uliopita tuzo ya amani ya Nobel ilichukuliwa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye makubaliano yake ya amani na Eritrea yalisitisha uhasama kufuatia vita vyao vya mpakani vya miaka ya 1998-2000.