Ikiwa ni miaka 30 tangu Mei 3 ya kila mwaka ilipotangazwa kuwa siku rasmi ya kuadhimisha Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD) na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka 1993, matukio mengi ya madhila dhidi ya uhuru wa waandishi na vyombo vya habari hapa nchini yameendelea kutotolewa taarifa.
Waandishi wa habari wamechukulia kukumbana na madhila kama unyanyaswaji, kupigwa, kunyang’anywa vifaa, na kutishiwa kama ‘ajali kazini’ na hivyo kutoyatolea taarifa. Msukumo wa taarifa umekuwa ukiwekwa kwenye matukio makubwa yanayohusisha kujeruhiwa, kutekwa ama kupoteza maisha; hivyo taarifa nyingi za madhila hazipo kwenye kumbukumbu.
Uanzishwaji wa Kanzidata na Malengo yake
Kutokana na changamoto hii, mwanzoni mwa mwaka 2012 Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilianzisha kanzidata ya kitaifa kwa ajili ya kurekodi madhila wanayopata waandishi wa habari ama vyombo vya habari. Lengo likiwa ni kuwa na ushahidi wa kitakwimu na uhalisia kwa ajili ya kufanya uchechemuzi wenye ushahidi.
Malengo mengine ni kutambua na kuwaumbua wanaonyanyasa na kuumiza wanahabari, ili kupata msaada wa kikanda na kimataifa, kuelimisha umma, kuwaambia waandishi wa habari kuwa kupatwa na madhila siyo ajali kazini na siyo changamoto za kitaaluma; na kuondoa kutokujali kwa wale wanaofanya madhila hayo.
Madhila yanayorekodiwa na MCT
Madhila yanayorekodiwa na kanzidata hiyo katika kipindi cha miaka kumi (2012 – 2022) ni kunyimwa taarifa, kutishiwa, kukamatwa, chombo cha habari kufungiwa, kutekwa, kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri, kupigwa faini kwa chombo cha habari, vifo, kuharibiwa vifaa vya kazi, kuondolewa katika eneo la tukio kinyume cha sheria na kujidhibiti (self-censorship).
Kanzidata hiyo imekuwa ikipokea taarifa zake kupitia vyombo vya habari, waandishi wa habari, waratibu wa klabu za waandishi wa habari na kupitia mitandao ya kijamii.
Idadi ya waandishi waliokumbwa na madhila
Katika kipindi cha miaka kumi toka kuanzishwa kwa kanzidata hiyo jumla ya waandishi wa habari 272, kati yake wanaume 219 na wanawake 53 walikumbwa na madhila mbali mbali kama yalivyoainishwa hapo juu na katika kipindi hicho hicho, vyombo vya habari 94 vilikumbwa na madhila hayo. Matamshi au vitendo 19 vilielekezwa kwa waandishi na vyombo vya Habari kwa ujumla.
Idadi ya madhila yaliyoripotiwa na kurekodiwa
Madhila ambayo yamerekodiwa katika kanzidata ya MCT katika kipindi hicho ni 271, ambapo kukamatwa kwa waandishi wa habari wakiwa kazini, kuliongoza kwa kuwa matukio 52, ikifuatiwa na vitisho kutoka kwa watoa taarifa mbali mbali matukio 50 na waandishi wa habari kunyimwa taarifa matukio 45.
Madhila mengine ni mashambulio ya mwili (assault) matukio 25, kufungiwa vyombo vya habari (29), faini (14), kuondolewa katika eneo la kazi au eneo la tukio kwa nguvu au kwa vitisho (10), kutekwa waandishi wa habari au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha matukio sita, kudhalilishwa matukio 13, na kujidhibiti kwa chombo cha habari matukio manne.
Pia kuna matukio 15 ya waandishi wa habari kuharibiwa na kutaifishwa vifaa vyao vya kazi, huku uminywaji wa mitandao ya kijamii matukio matatu, mauaji matukio matatu, na kuingilia uhuru wa uhariri matukio mawili.
Wahusika wa matukio hayo
Kanzidata inaonyesha kuwa taasisi iliyoongoza kwa matukio mengi dhidi ya uhuru wa habari ilikuwa ni polisi ambayo ilikuwa na matukio 51.
Wahusika wengine ni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) matukio 21, wizara mbali mbali matukio 14, wakuu wa wilaya matukio tisa, mashabiki wa mpira matukio matano, wakulima na wafugaji matukio mawili na watu wasiojulikana matukio kumi. Idara ya Habari Maelezo (Bara) haikubaki nyuma nayo ilikuwa na matukio nane na wakuu wa mikoa matukio saba.
Wahusika wengine wa madhila yaliyowapata waandishi wa habari katika kipindi hicho ni mgambo, madiwani na watendaji kata matukio manne, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) matukio matatu, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) matukio matatu, mahakama matukio matatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), matukio mawili, Chama cha Mapinduzi (CCM) tukio moja, Tume ya Utangazaji Zanzibar matukio mawili, maafisa maendeleo ya jamii matukio mawili na Mwananchi Communications Limited matukio mawili.
Wahusika wafuatao wamefungana kwa kuwa na tukio moja moja, nao ni viongozi wa dini, Azam Media Group, wapiga kura wa Msikiti wa Makanyagio, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Matukio hayo yalitokea wapi
Katika mikoa 26 ya Tanzania Bara madhila kwa uhuru wa habari yaliyorekodiwa yalitokea katika mikoa 25. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa katika kipindi hicho cha miaka kumi, mkoa wa Songwe haukuwa na madhila.
Ifuatayo ni mikoa kumi ya Tanzania Bara iliyoongoza kwa madhila na idadi yake. Mkoa wenye matukio mengi zaidi ni Dar es Salaam matukio 43, Shinyanga (18), Arusha (17), Dodoma (15), Mara (13), Kagera (12), Kilimanjaro (11), Tanga (10), Ruvuma na Singida matukio nane kila mmoja; na Mwanza, Rukwa na Pwani matukio saba kila mmoja. Kwa upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba), jumla ya madhila 15 yaliripotiwa katika kipindi hicho.
Taarifa ya idadi ya madhila iko kama ifuatavyo 2013 (38), 2014 (27), 2015 (20), 2016 (32), 2017 (5), 2018 (24), 2019 (40), 2020 (41), 2021 (26) na 2022 (18).
Kutokea kwa madhila kumeendelea kujenga hofu miongoni mwa waandishi wa habari na vyombo vya habari na kusababisha uandishi wa habari usio wa kina na kukosekana kwa habari za kiuchunguzi.
Matukio haya pia yameendelea kuishusha Tanzania katika sura ya kimataifa. Kwa mfano, katika ripoti za World Press Freedom Index, Tanzania imeendelea kushuka katika viwango vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 70 mwaka 2013 mpaka nafasi ya 124 mwaka 2021 na mwaka 2022 nafasi ya 123.
Wito kwa wanahabari
MCT inawahimiza waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru, weledi na kufuata maadili, na pale kunapokuwa na changamoto kuwasiliana na Baraza. Madhila kwa waandishi wa habari yasichukuliwe kama ni ‘ajali kazini’, bali ni mambo yanayotakiwa kuripotiwa na kurekodiwa ili Tanzania iwe na rekodi ya madhila ambayo waandishi wanakutana nayo. Uwepo wa taarifa utasaidia kuonyesha ukubwa wa tatizo na kuongezwa kwa jitihada za kutafuta suluhu. Jitihada hizi zitakuwa na mashiko zaidi pale kunapokuwa na ushahidi wa kitakwimu.
Waandishi wa habari na taasisi za kihabari ziendelee kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha tasnia ya habari inafanya kazi kwa uhuru lakini kwa kufuata maadili na kwa weledi.
Pia MCT inawahimiza waandishi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata kanuni za maadili ya uandishi wa habari ambayo tumejiwekea wenyewe ili yaendelee kuongoza katika utendaji wetu na namna tunavyoandika habari zetu.
Ni jukumu la kila mwandishi kuhakikisha anaripoti matukio yote ya kumdhalilisha au kumsababisha asiweze kufanya kazi zake kwa uhuru na weledi. Tafadhali ripoti matukio hayo MCT au Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa hatua zaidi.
Wakati huo huo tunazikumbusha taasisi na watendaji mbalimbali kuwa haki ya kupata taarifa na habari ni haki ya kikatiba kwa wananchi wa Tanzania. Kukwaza uhuru wa habari pasipo sababu halali ni kuwanyima wananchi haki yao.
Taarifa hizi pia zinapatikana kwenye kanzidata ya MCT www.pressviolation.or.tz au kwenye ripoti za UTPC ambazo pia zinapatikana katika tovuti ya www.utpc.or.tz au tembelea ofisi hizo kwa taarifa zaidi.
Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji – MCT