Wizara ya Nishati kupitia kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC imesema Serikali imewasimamisha kazi Mameneja wa Kampuni ya TANOIL – Kampuni Tanzu ya TPDC, inayojihusisha na biashara ya mafuta.

Taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya Habari, imesema kabla ya uamuzi huo Serikali kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, ilielekeza kufanyike ukaguzi wa kina wa uendeshaji wa kampuni ya TANOIL uliofanywa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali uliobaini viashiria vya ubadhirifu mkubwa katika uendeshaji wa Taasisi hiyo.

Wizara imewataja waliosimamishwa kuwa ni Meneja Mkuu, Mhandisi. Kapuulya Musomba, Meneja wa Fedha na Utawala, James Batamuzi, Meneja wa Hifadhi ya Mafuta, Sudi Abdalla na Meneja wa Usambazaji na Uendeshaji, Amour Marine.

Kufuatia hatua hiyo, Serikali kupitia Bodi ya TPDC, imeweka uongozi wa muda wa kuendesha shughuli za Kampuni hiyo na kuiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kwa hatua stahiki.

Aidha, Bodi ya TPDC pia imeanza kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo ya kuongeza udhibiti na kuandaa mkakati mpya wa kibiashara wa TANOIL.

Hata hivyo, mwezi uliopita (Machi, 2023), Serikali ilibadilisha menejimenti ya TPDC katika jitihada za kuimarisha uendeshaji wa Shirika ikiwemo usimamizi wa kampuni tanzu za Shirika.

Ongeza kipato kusanya mgao wa Tsh 5m kutoka Meridianbet
Serikali yafafanua utekelezaji athari za kiuchumi, kijamii