Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sekta ya Ujenzi imefanikisha zoezi la kuwapeleka watumishi 44 kushiriki mafunzo kwa vitendo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Injinia Elius Mwakalinga wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo kwa vitendo kazini ambapo amesisitiza kwa watumishi hao kujifunza kwa manufaa ya Sekta ya Ujenzi na Taifa kwa ujumla ili kujenga uchumi wa viwanda na hivyo kufanikisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Wote tunafahamu kuwa hivi sasa ni takribani miaka zaidi ya 50 tokea tupate uhuru lakini miradi mingi inaendelea kutekelezwa na wageni hivyo basi mtumie fursa hii mliyopewa kuwa mabalozi wazuri ili nchi iweze kutengeneza makandarasi na washauri elekezi wazawa wengi miaka ya baadae,”amesema Mwakalinga.

Aidha, amewataka watumishi hao kuwa na nidhamu wakiwa katika maeneo yao ya mafunzo na kutokuwa wajuaji bali waongeze ujuzi kwa yale wanayoyajua na kujifunza kwa bidii teknolojia mpya ambazo walikuwa hawazitumii.

Amefafanua kuwa mpango huo utafanyika kwa kipindi cha miezi sita sita na ni moja kati ya mipango ya Wizara iliyojiwekea katika kuhakikisha inaleta chachu ya maendeleo ya nchi hasa katika suala zima la usimamizi na ujenzi wa miundombinu bora.

Kwa upande wake Mtaalam wa Utafiti kutoka Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB) Injinia Neema Fuime, amesema kuwa mafunzo hayo ya watumishi kwa vitendo wakiwa kazini itasaidia fedha nyingi zinazotolewa kwenda kwa makandarasi wageni kubaki hapa nchini na thamani ya fedha kuonekana kwa kuwa wasimamizi na washauri watakuwa ni wazawa wenye uchungu wa nchi yao.

Naye Mkadiriaji Majengo kutoka Bodi ya Usajili na wakadiriaji Majenzi (AQRB), Joseph Ringo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara kwa kutoa fursa hiyo kwa watumishi na kumuahidi Katibu Mkuu huyo kushirikiana kikamilifu na wataalam hao na ameahidi kutoiangusha Serikali iliyowaamini katika na kuwapeleka kwenye miradi mikubwa ya kitaifa katika suala la usimamizi, ujenzi na ushauri.

 

DJ Arafat afariki dunia kwa ajali ya pikipiki, daktari aeleza hali ilivyokuwa
DC aamuru wachimbaji wa madini kuswekwa ndani