Wizara ya Nishati na Madini imekanusha taarifa kuwa Waziri wake Prof. Sospeter Muhongo, katika kikao chake na Benki ya Dunia (WB), kilichofanyika Septemba 28 mwaka jana kilikuwa cha kujadili mchakato wa kupandisha bei ya umeme nchini.
Aidha, katika taarifa ya kikao hicho Wizara imesema kuwa walijadili upatikanaji wa umeme wa kutosha, uhakika na bei nafuu kwaajili ya kuchochea shughuli za maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi, kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) na kupunguza deni la Tanesco.
Hata hivyo, Wizara hiyo imesema kuwa wamekuwa wakifanya vikao na wadau mbalimbali na Taasisi za Umma, Binafsi na washirika wa Maendeleo yakiwemo Mashirika ya Kifedha ya Kimataifa kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya Nishati na Madini.
Katika taarifa hiyo, Wizara imeongeza kuwa kikao hicho kilihudhuriwa na taasisi nyingine zikiwemo Wakala wa Nishati na Vijijini (REA), Shirika la Madini la Taifa(STAMICO), Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania(TPDC), Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).