Serikali nchini, imeiagiza Wizara ya Afya kuendelee kuhamasisha taasisi na wadau kuchangia maeneo muhimu na utatuzi wa changamoto za jamii katika sekta ya afya kutokana na akina mama kusumbuliwa na tatizo la fistula na wengi wao kupoteza matumaini kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Oktoba Mosi, 2022 mara baada ya kuhitimishwa kwa mbio za hisani jijini Dar es Salaam na kusema pamoja na jitihada za Serikali kutoa huduma, bado inahitaji kuungwa mkono na Watanzania ili kunusuru maisha ya akina mama.
Amesema, “Suala la kuchangia maendeleo na utatuzi wa changamoto za jamii ni la Watanzania wote tukishirikiana, tutaifanya Tanzania kuwa salama, nitoe rai kwa makampuni mengine yanayofanya biashara nchini kushirikiana na Serikali ili tutatue changamoto hizo.”
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna alisema takwimu zilizopo zinaonesha wanawake 10,000 wana fistula na kila mwaka wanaongezeka 3,000 lakini wanaopata matibabu ni 1,300 huku gharama ya kumtibu kila mmoja zikiwa ni shilingi milioni 4.
Amesema, “Ili kuchangia matibabu ya wanawake wenye tatizo la fistula, mwaka jana waliweka lengo la kukusanya shilingi . bilioni moja kwa kipindi cha miaka minne, lakini wamelitimiza ndani ya miaka miwili, ambapo katika mbio za leo Viongozi walioshiriki ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuberi Ali Maulid na Naibu Spika, Mussa Azzan Zungu.
Wengine ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Shaka Hamdu Shaka, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Godwin Gondwe, Mameya wa Dar es Salaam na Zanzibar, Wabunge wa Ukonga na Kibamba, wakurugenzi wa taasisi na mashirika mbalimbali.