Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limewaagiza Mabingwa wa Soka Barani Afrika Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, kumlipa Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania Simon Msuva zaidi ya dola za Kimarekani laki saba ‘700,000’ (Zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6 za Tanzania).
FIFA imetoa agizo hilo kwa Wydad Casablanca, baada ya kukamilisha kesi iliyokuwa inaunguruma baina ya pande hizo mbili kwa zaidi ya miezi sita.
Hata hivyo Wydad Casablanca ndio ilikua ya kwanza kufungua kesi dhidi ya Msuva, ikiamini Mchezaji huyo alikua na jambo la kujibu kwa madai alivunja mkataba bila sababu, lakini mambo yamewageukia na wametakiwa kumlipa stahiki zake.
Baadae Msuva aliifungulia Mashtaka Wydad Casablanca, kwa kushinikiza kulipwa stahiki zake, ambazo hakuzipata kwa muda mrefu kutoka kwa miamba hiyo ya Afrika.
Msuva alisaini mkataba wa miaka minne na Klabu hiyo ya Casablanca, alilazimika kuusitisha mkataba huo mwezi Disemba mwaka 2021, kutokana na malimbikizo ya mishahara pamoja na pesa za usajili (signing fee).