Timu ya Yanga leo imeshuka dimbani mara ya pili katika mchezo wake wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara ambapo ilikua ikichuana na Polisi Tanzania ambapo mchezo huo uliisha kwa sare ya mabao 3-3 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mchezo wenyewe ulikua wa vuta nikuvute ambapo Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 6 kupitia mshambuliaji wao Mrisho Ngassa baada ya kupewa pasi na beki wa kulia, Juma Abdul aliyeipiga kutoka kulia mwa uwanja.
Na katika dakika ya 34 kipindi cha kwanza timu ya Polisi ilisawazisha bao hilo kupitia mchezaji wake Ditram Nchimbi ambapo mpaka dakika 45 za kwanza zilimalizika kwa matokeo ya sare kati ya timu hizo mbili.
Kipindi cha pili Polisi walipata bao la pili kupitia kwa Nchimbi aliyefunga baada ya kupokea pasi iliyopenyezwa katikati mwa uwanja kumfunga kiufundi kipa Metacha Mnata ikiwa ni dakika ya 55 pia katika dakika ya 58 tena, Nchimbi alifunga tena kwa mpira wa kichwa na kufanya matokeo yawe 3-1.
Yanga waliamka tena ambapo David Molinga ‘Falcao’ alifunga katika dakika ya 65 baada ya kipa wa Polisi, Kulwa Manzi kushindwa kuumiliki mpira vizuri baada ya kumponyoka na kuelekea nyavuni pia mnamo dakika ya 69 tena, Molinga aliingia tena kambani kupitia mpira wa faulo ambao ulimzidi nguvu kipa wa Polisi, na mpaka kipyenga kinamalizika, matokeo ni 3-3.