Klabu ya Young Africans SC imetangaza kusaini Mkataba Mpya na Kampuni ya Michezo ya kubashiri ya SportPesa kwa Mkataba wenye thamani ya Shilingi Bilioni 12, leo Jumatano (Julai 27) jijini Dar es salaam.
Young Africans imetangaza dili hilo, baada ya kampuni ya SportsPesa kuachana na Simba SC, siku kadhaa zilizopita, kufuatia mkataba wa awali kufikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2021/22.
Mkataba mpya wa Young Africans na Kampuni utadumu kwa muda wa miaka mitatu, wenye thamani ya Shilingi Bilioni nne za kitanzania kila mwaka.
Mkataba huo unakua wa gharama zaidi katika klabu ya Young Africans tangu ilipoanza kudhaminiwa na Kampuni ya SportsPesa, ambapo awali udhamini huo ulikuwa pia upande wa watani zao wa jadi Simba SC.
Kwa sasa Simba SC inadhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya kubashiri ya M-bet kwa muda wa miaka mitano.
Udhamini wa Simba SC na Kampuni hiyo unathamani ya Shilingi Bilioni 15, ambapo kila mwaka Klabu hiyo itapata Shilingi Bilioni 3.