Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC wameendelea kushikilia msimamo wa kutokua tayari kumuachia Mshambuliaji wao kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati Ceser Manzoki, ambaye anawaniwa na Simba SC ya Tanzania.

Mshambuliaji huyo mzaliwa wa DR Congo alimaliza Ligi Kuu ya Uganda msimu uliopita akiwa mfungaji Bora, hali ambayo iliwavutia viongozi wa Simba SC kumshawishi kujiunga nao msimu huu, lakini dili limekwama mezani kwa viongozi wa Vipers SC.

Taarifa kutoka Uganda zinaeleza kuwa, Uongozi wa Vipers SC umeitaka klabu ya Simba SC kununua mkataba wa Mshambuliaji huyo uliosaliwa na muda wa miezi miwili, kwa thamini ya Dola za Kimarekani 200,000 (Sawa na Shilingi milioni 450).

Hata hivyo Uongozi wa Simba SC umesema haupo tayari kutoa pesa hizo, kutokana na muda wa mkataba wa Manziki kuwa mdogo, lakini umeendelea kukaa katika meza ya mazungumzo ili kuipata saini ya Manzoki kabla ya Dirisha la usajili halijafungwa kati kati ya mwezi ujao.

“Tunapambana kuona kama tunaweza kumpata kabla dirisha la usajili wa CAF halijafungwa Agosti 15 ikishindikana hapo basi itabidi tusubiri hadi Dirisha Dogo, tumchukue kama mchezaji huru.”

“Pesa wanayoitaka ni nyingi na mchezaji amebakiza mkataba wa miezi miwili, shida ipo hapo, wamekomaa walipwe Dola 200,000 ambayo ni pesa nyingi mno, ila ngoja tuone mazungumzo yatakavyoisha na ikishindikana basi tutamchukua Desemba,” amesema kiongozi wa Simba SC.

Manzoki alikuwa sehemu ya wachezaji waliotajwa awali kuwa huenda wangejiunga na Simba SC katika kipindi hiki cha Usajili wa kuelekea msimu mpya, lakini mambo yanaendelea kuwa magumu kukamilisha ndoto zake za kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Geita Gold FC yamvuta Wawa Kimataifa
Young Africans, SportPesa zasaini mkataba mpya