Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umesema upo tayari kuona kikosi chao kikipangwa na timu yoyote katika Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Tambo hizo za Uongozi wa Klabu hiyo nguli katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zimekuja baada ya kikosi cha Young Africans kujihakikishia kucheza Robo Fainali, kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya US Monastir juzi Jumapili (Machi 19).
Afisa habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema kutokana na ubora wa kikosi chao kwa sasa, hawana hofu ya kukutana na timu yoyote katika Michuano hiyo, ambayo imebakisha mchezo mmoja ili kuhitimisha Hatua ya Makundi.
“Kwa kikosi chetu cha sasa, hakuna timu kwa Afrika ambayo tunaihofia ila kwa sasa wapinzani wetu ambao wanakuja wanatuhofia.”
“Sisi hakuna timu Afrika kwenye Kombe la Shirikisho ambayo tunaihofia, hata US Monastir walikuwa wanatuhofia, ASEC, Rivers, Pyramids wote wanatuwaza.”
“Yoyote anayekuja sisi tunamalizana naye na tunaamini kwamba kwenye hatua ya robo fainali tutafanya vizuri na kutinga hatua ya nusu fainali.” Amesema Ally Kamwe
Kwa sasa Young Africans inaongoza Kundi D na inaweza kukutana na Marumo Gallants (Afrika Kusini), USM Alger (Algeria), Saint-Éloi Lupopo (DR Congo) au Al Akhdar (Libya) zilizopo Kundi A, za Kundi B ni Rivers United (Nigeria) na ASEC Mimosas (Ivory Coast) au zile za Kundi Kundi C, ASFAR (Morocco), Pyramids na Future (Misri).