Kikosi cha Young Africans kimeingia kambini leo Ijumaa kujiandaa na mchezo wa ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, ambao utapigwa Jumapili, Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Afisa Habari wa Young Africans Hassan Bumbuli amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri kueleka mchezo huo, ambao utaamua nanai atakaa kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans ipo nafasi ya tatu kwa kufikisha anama 55, ikitanguliwa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kumiliki alama 57 huku Simba SC wakiwa kileleni kwa alama 72.
“Tumerejea salama kutoka Dodoma, wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanatarajia kuingia kambini leo”
“Tunashukuru hatuna majeruhi, Morrison tayari ameungana na wachezaji wengine, nahodha wetu Papy Tshishimbi leo atafanyiwa vipimo kubaini utayari wake kuelekea mchezo wa Azam,” amesema
“Tunawaita mashabiki wetu waje kwa wingi kushuhudia burudani. Tunahitaji ushindi, sapoti yao itawapa hamasa wachezaji. Tulipoteza mchezo wa kwanza dhidi yao lakini hawajawahi kutufunga mara mbili hivyo mashabiki waje kwa wingi kushangilia ushindi”
Kwenye mchezo huo Young Africans watamkosa beki kutoka Ghana Lamine Moro, anaetumikia adhabu ya kadi nyekundi, aliyoipata katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa mjini Dodoma, Uwanja wa Jamuhuri Juzi Jumatano.