Uongozi wa Young Africans umesema mabingwa wa soka Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC wajiandae kulipa Shilingi milioni 600 endapo watapata ushindi katika malalamiko yao dhidi ya kiungo kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, ambayo tayari wameyawasilisha Mahakama ya Usululishi ya Michezo (CAF).
Mwenyekiti wa Young Africans, Mshindo Mbette Msolla amesema hatua ya kudai fidia kubwa dhidi ya Simba SC imelenga kukomesha masuala kama hayo katika soka nchini.
Msolla amesema suala la wao kushinda katika kesi hiyo ni la kawaida kutokana na jinsi sakata hilo lilivyoamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF).
“Katika hili hatutanii na ndiyo maana tumelipeleka mbele ya vyombo vya sheria vya kimataifa, tunajua nini tunachokifanya ndiyo maana tumeamua kuchukua hatua stahiki,” amesema Msolla.
Juzi Young Africans ilisema haiwezi kutoa kibali cha kazi cha winga Bernard Morrison kwani ni mchezaji wao halali, hivyo wanaishangaa Wizara ya Kazi kuwalazimisha kutoa kibali hicho.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Young Africans, Hassan Bumbuli alisema wana mkataba na Morrison hivyo hawaoni haja ya kurudisha kibali cha kazi cha mchezaji huyo wakati bado wana kesi nae.
“Sisi hatujakizuia ila tunacho kibali chake cha kazi. Wamekuja Wizara ya Kazi wameleta barua wakitaka turudishe kile kibali ila tumewajibu hatuwezi kufanya hivyo, kwani Morrison ni mchezaji wetu tuna mkataba naye na tuna shauri nae.”
“Tunashangaa wameshapita makocha hapa wameondoka na hatujawahi kuulizwa na Serikali kuhusu kurudisha vibali, huwa tunarudisha wenyewe, sasa iweje kwa Morrison, ana ushawishi gani?” alisema
“Hatujazuia wala hatuna sababu ya kuzuia kwani hata Simba wametuomba uhamisho wa Morrison kwa njia ya barua na njia ya mtandao na tumewaambia kuwa huyu hatujamalizana nae,”
Morrison ambaye aliichezea Young Africans msimu uliopita amezua utata mkubwa wa usajili baada ya kusaini kwa mabingwa wa Tanzania bara na kombe la Shirikisho Simba SC.
Mchezaji huyo alikana kusaini mkataba mpya na Young Africans na kudai saini yake imeghushiwa, na alipeleka malalamiko kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Elias Mwanjala ilimpa ushindi Morrison wakidai kweli mkataba halisi wa mchezaji huyo ulikuwa na saini moja tu ya viongozi wa Young Africans na haukuwa na saini ya mchezaji huyo, hivyo kumruhusu kucheza timu yeyote.
Wakati hukumu hiyo ikitoka, tayari Morrison alikuwa amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba na ametambulishwa rasmi wakati wa Simba Day kuwa miongoni mwa nyota watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajia kuanza Septemba 6 mwaka huu.