Kikosi cha Young Africans kimeondoka Dar es salaam kuelekea mjini Unguja Visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo tayari imeshaanza kutimua vumbi katika Uwanja wa Amaan.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, amesema kikosi chote cha wachezaji wa klabu hiyo kimekwenda huko na kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Cedric Kaze.
“Kikosi kimeondoka leo kwenda Zanzibar, ambaye hatokuwapo ni Kocha Mkuu Nasreddine Nabi kutokana na kuwa na udhuru, lakini Kaze yeye atakuwapo kusimamia timu, kwa hiyo wanachama na mashabiki wa Young Africans mjini Zanzibar wasiwe na wasiwasi kwani wachezaji wote watawaona,” amesema Bumbuli.
Mwaka jana (2021), Young Africans ilitwaa Ubingwa wa Michuano hiyo kwa kuwafunga watani zao wa jadi Simba SC kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar kwa mikwaju ya Penati 4-3, baada ya kutoka suluhu kwa dakika 90 za mchezo.
Young Africans itaanza kampeni yake ya kutetea Ubingwa wa Mapinduzi CUP kesho Jumatano (Januari 05) majira ya saa 2:15 usiku itakapocheza dhidi ya Taifa Jang’ombe kwenye Uwanja wa Amaan.
Mchezo huo utatanguliwa na watani zao wa jadi, Simba SC ambao watacheza saa 10:15 alasiri kwenye uwanja huo huo dhidi ya Selem View.