Uongozi wa klabu ya Young Africans umeanza maandalizi na mipango ya kuhakikisha msimu ujao wanatisha zaidi, baada ya kufanya vizuri katika michuano ya ndani na nje ya Tanzania msimu huu 2022/23.
Young Africans wamekuwa bora baada ya kufanikiwa kutinga Fainali Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini jumal ya mabao 4-1, baada ya mchezo wa nyumbani na ugenini.
Katika michuano ya ndani, Young Africans imetangazwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara zikisalia mechi mbili, huku mwanzoni mwa msimu ikibeba Ngao ya Jamii, pia ipo Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Rais wa Young Africans Injinia Hers Said, amesema wanatambua ubora ambao kikosi chao umekionesha katika michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo wameanza kuweka mipango kwa ajili ya msimu ujao kuufikia ubora mkubwa zaidi.
“Kwanza niwapongeze benchi la ufundi, wachezeaji wetu na mashabiki, bila kusahau viongozi wenzangu, kwa pamoja nguzo hizi zimekuwa muhimu sana katika haya mafanikio.
“Kikubwa ni kwamba tunatambua kuwa msimu ujao utakuwa tofauti na msimu huu, hivyo tayari tumeshaanza maandalizi ya msimu mpya kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vema kwa kuzingatia mashindo makubwa ambayo tutakwenda kushiriki ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesemakiongozi huyo.
Tayari kikosi cha Young Africans kimeshaanza safari ya kurejea nchini Tanzania, kikitokea Afrika Kusini baada ya kumaliza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants.