Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said amesema kuwa hakuna timu ya kuwazuia kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwani kikosi chao kina Benchi Bora la Ufundi na Wachezaji wenye ubora ambao wanaweza kufanya jambo lolote kubwa.

Kauli hiyo ya Hersi inakuja baada ya kikosi cha Young Africans kuibuka na ushindi wa 2-0 katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Rivers United uliopigwa Jumapili (April 23) nchini Nigeria.

Hersi amesema kwa namna ambavyo timu hiyo inavyokwenda kuna kila dalili kuwa watakwenda hadi fainali kwa sababu makocha wao wameshabadilisha mtazamo wa hatua ya makundi na sasa wanaona kuna neema zaidi mbele yao.

“Sisi ni wadogo, tumeikuta hii klabu, na malengo yetu ni kuchukua ubingwa kwenye mashindano yoyote tunayoshiriki. Sishangai kuona malengo yetu kwenye mashindano ya kimataifa yanaanza kukomaa.ā€

“Young Africans haikuwa kwenye nafasi nzuri katika mashindano ya kimataifa, lakini sasa imethubutu na tumefika makundi na kumaliza nafasi ya kwanza, baada ya hapo tukaingia Robo Fainali, tumeshinda mchezo wetu wa kwanza ugenini, tuna faida ya mabao mawili na mchezo ujayo tutakuwa nyumbani.ā€

“Njia ya nusu fainali tunaiona ni nyeupe, ukivuka huko chochote kinaweza kutokea, kwa nini isiwe Young Africans ikapata nafasi ya kuchukua ubingwa huu wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika? Itakuwa furaha kwa mashabiki, viongozi na Tanzania kwa ujumla. Naona Young Africans wakiwa mabingwa kabisa,” amesema kiongozi huyo

Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria Jumapili (April 30), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Young Africans itapaswa kulinda ushindi wake wa mabao 2-0 ama kusaka ushindi mwingine, huku Rivers United ikitakiwa kusaka ushindi wa mabao 3-0 na kuendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Nusu Fainali ya Michuano hiyo.

Hotel yazindua huduma ya kujiuwa kwa waliochoka kuishi
Young Africans kurudi kambini leo