Meneja wa Klabu ya Young Africans Walter Harrison amesema maandalizi yao kuelekea mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ dhidi ya Marumo Gallants yanaendelea vizuri na wachezaji wote wapo katika hali nzuri.

Young Africans iliwasili katika mji wa Rustenburg, Afrika Kusini juzi Jumapili (Mei 14) mchana na kulakiwa na Balozi wa Tanzania, Gaudence Milanzi na Watanzania waishio nchini humo wakiwemo mashabiki wa watani zao Simba.

Walter amesema kikosi chao kilianza mazoezi jana Jumatatu (Mei 15) asubuhi kwenye uwanja unaomilikiwa na hoteli waliyofikia na leo jioni ndio watakwenda kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Royal Bafokeng utakaochezewa mchezo huo.

“Wachezaji wote tuliokuja nao wapo katika hali nzuri kiafya na benchi letu la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi linaendelea na ratiba yake kama kawaida ya kuiandaa timu kuhakikisha tunapata kile kilichotuleta huku,” amesema Walter

Kwa mujibu wa Walter, Nabi amekuwa akizungumza na wachezaji akimtaka kila atakayepata nafasi kucheza kwa jihadi na kujituma kwa nguvu zake zote kama walivyofanya kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza.

“Tunatakiwa kuipigania heshima ya klabu yetu kwa kucheza kama wanajeshi, tunatakiwa kwenda kuipigania Young Africans, tunatakiwa kwenda kuipigania Tanzania, natamani kuona kila mchezaji akicheza kwa jihadi na kujitolea nguvu zake zote,” amesema Nabi.

Katika mchezo huo, Young Africans inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kutinga Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, hiyo ni baada ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam juma lililopita.

Ibrahim Mutaz kuamua Nusu Fainali CAF CC
Wafanyabiashara wakubaliana na Waziri Mkuu