Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umewasilisha mashataka dhidi ya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei toto’ katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’.

Fei Toto aliyejiunga na Young Africans Agosti 15-2018 akitokea JKU ya Zanzibar, kabla ya kutimka Kambini mkataba wake klabuni hapo ulitarajiwa kumalizika Mei 30-2024.

Chanzo cha Habari kutoka Young Africans kinaeleza kuwa Uongozi wa Klabu hiyo kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu Andre Mtine, umewasilisha Barua ya mashtaka kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ili wamuite Fei Toto kwa ajili ya kuzungumzia sakata lake la kuondoka Kambini na kutaka kuvunja Mkataba.

“Tayari Young Africans wameshawasilisha Barua kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF wakiomba Fei Toto aitwe ili waweze kuzungumzia sakata lake hilo la kutoroka kambini na kuomba kuvunja mkataba kinyume na utaratibu.”

“Tayari Barua imeshatumwa TFF na wamethibitisha kuipokea na kumfahamisha Fei Toto, hivyo tunaamini ndani ya juma hili ataitwa ili akajieleze nini kilichomfanya atoroke na kuvunja mkataba kinyemela.”

“Kama hatakuwa na sababu za msingi basi kuna uwezekano mkubwa sana wa kuadhibiwa.” kimeeleza chanzo cha Habari kutoka Young Africans.

Desemba 23-2022 zilitoka taarifa za Fei toto kuandika Barua ya kuvunja Mkataba wake ndani ya Klabu ya Young Africans, ambapo tangu hapo hajaonekana kambini akitimkia kwao Zanzibar kabla ya hivi karibuni kusafiri kwenda Dubai kwa mapumziko.

Viongozi vyama vya Siasa watinga Ikulu
Wabunge wa upinzani jela miezi sita kwa shambulio