Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amezungumzia namna ubora wa wachezaji wa Young Africans unavyowaumiza kichwa wanapokwenda kukutana kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Singida BS imepoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Bara ikianza na Young Africans ikifungwa mabao 2-0 pamoja na ule wa KMC waliofungwa mabao 2-0.
Jumapili (Mei 21), Singida BS wataikaribisha Young Africans kwenye Uwanja CCM Liti, mkoani Singida, hivyo wana mtihani mkubwa wa kuifunga Young Africans ambao tayari ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara.
Pluijm amesema kucheza na timu kama Young Africans inakubidi utumie mbinu za hali ya juu ili uweze kuwafunga.
Amesema kwa upande wa wachezaji hawatakiwi kurudia makosa ili kushinda mchezo huu, kwani lolote linaweza kutokea kama wakiamua kushinda au kushindwa.
“Michezo iliyopita ikiwemo na KMC tulishindwa kwani kuna baadhi ya wachezaji niliwapumzisha ndio maana niliwachezesha baadhi yao nafasi nyingi na wengine kuwa na kadi za njano,”
“Tunakwenda kucheza kwa nguvu na ubora wote bila kupoteza nafasi kama mchezo uliopita dhidi yao hivyo tutabadilisha mambo.”