Klabu ya Young Africans inahusishwa na mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa pembeni wa Azam FC Iddy Seleman Nado, ambaye mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu 2020/21.
Young Africans inatajwa kujipanga kufanya usajili wa mshambuliaji huyo, kufuatia mikakati waliojiwekea ya kuwa na kikosi bora kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na michuano ya kimataifa endapo watapata nafasi ya kushiriki.
Mmoja wa viongozi wa Young Africans ambaye hakutaka jina lake lianikwe hadharani amesema, wameshaanza mipango na mikakati ya kumsajili mshambuliaji huyo, na wanamini watafanikiwa.
“Tunapambana naye tuweze kumchukua wakati huu, shida naona kama yeye na meneja wake wanaongea na sisi huku wanaongea pia na Azam, ila hatutakata tamaa,” amesema kiongozi huyo.
“Tukimpata Nado itakuwa safi kwa kuwa tutakuwa tumelinda nafasi ya wachezaji wa kigeni kwa kuwa na mtu wa maana kutoka ndani, unajua msimu huu Nado amekuwa na kiwango bora sana tunachopenda sio mtu wa kukata tamaa.”
Hata hivyo, taarifa kutoka Azam FC zinaeleza kuwa, Iddy Nado ameshaanza mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kusaini mkataba mpya, kufautria kumvutia kocha George Lwandamina.
Nado alisajiliwa Azam FC msimu miwiwli iliyopita wakati wa utawala wa kocha Ettiene Ndayiragije akitokea Mbeya City FC, ambako alifanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa wakati huo.