Kikosi cha Young Africans kimerejea kambini kuanza maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Young Africans imerejea Kambini baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, uliomalizika kwa Wananchi kupigwa mabao 2-0, Jumapili (April 16) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mbali na kuanza maandalizi ya kukabili Rivers United, Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kesho Alhamis (April 20), kuelekea Nigeria.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema kikosi hicho kimeanza mazoezi kikiwa na tafakari juu ya mchezo unaokuja wakitaka kurekebisha makosa ya mchezo uliopita wakiwa na ari ya kutafuta ushindi ugenini.

“Kulingana na ratiba ilivyo, tutaondoka kuelekea Nigeria kwa ajili ya maandalizi ya mwisho tukiwa kule dhidi ya Rivers, matokeo yaliyopita hata wachezaji wanafahamu hayakuwa mazuri kulingana na ukubwa wa mchezo wenyewe na wanajiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi ijayo tupate matokeo mazuri,” amesema Kamwe

Young Africans itakipiga na Rivers United Jumapili (April 23) saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Taifa wa Godswill Akpabio, Akwa Ibom.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Nasreddine Nabi inaivaa Rivers ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na kufurushwa kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita kwa kufungwa kwa kipigo cha bao 1-0 katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.

Biteko ahimiza mshikamano, udumishaji wa amani
Kipyenga Uchaguzi TPBRC chapulizwa