Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans limekirudisha ‘Gym’ kikosi chake kwa lengo la kuongeza stamina na kutafuta pumzi ya kutosha.
Jumanne (Januari 17) Kocha wa Young Africans Nasreddin Nabi alikipeleka kikosi chake katika ‘Gym’ za Gymkhana jijini Dar es salaam kabla ya kurudi Uwanjani kwa siku mbili kwa ajili ya mazoezi.
Kocha Nabi amesema aliamua kikosi chake kurudi ‘Gym’ ili wachezaji wawe na pumzi ya kutosha kuhakikisha wanaweza kustahamili dakika 90 bila kuchoka.
Robertinho: Hakuna kama Mgunda, Matola
“Sio kwamba hawakuwa na pumzi, ni katika harakati za kuboresha kikosi kwa kuwa tunahitaji kufanya vizuri, tunatakiwa kutafuta mbinu mbalimbali za kumudu mapambano.” amsema kocha huyo kutoka Tunisia
Kocha huyo amesema leo Jumamosi na Kesho Jumapili, watafanya mazoezi ya Uwanjani ili kujiweka sawa kuhakikisha wanaendelea wimbi la ushindi dhidi ya Ruvu Shooting keshokutwa Jumatatu (Januari 23).
Katika hatua nyingine Nabi amesema, kikosi chake kimekamilika baada ya wachezaji ambao walikuwa mapumziko kurejea na kuungana na wenzao.
Wachezaji ambao walikua hawajajiunga na wenzao na wamerejea ni Bernard Morrison, Yannick Bangala na Stephen Aziz Ki.
Pia kiungo Khalid Aucho ambaye alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, jana Ijumaa (Januari 20) alianza mazoezi na wenzake baada ua kupona majereha hayo.