Uongozi na Wachezaji Young Africans mapema hii leo wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wanafunzi wa Shule ya Mazoezi Mwenge, Tabora Mjini ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.
Young Africans ipo mjini Tabora, kwa ajili ya mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), utakaowakutanisha dhidi ya Biashara United Mara, kesho Ijumaa (Juni 25).
Uongozi na Wachezaji wa klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ulifika shuleni hapo na kuzungumza na uongozi wa Shule, na baadae ulitoa msaada wa vitu mbalimbai kwa ajili ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine Uongozi na Wachezaji wa Young Africans wametembelea kituo cha kulelea watoto Yatima Cha IGAMBILO ISLAMIC OPHANS CENTER kilichopo Mjini Tabora na kutoa msaada wa vyakula.
Young Africans iliwasili mjini Tabora jana Jumatano (Juni 23) majira ya asubuhi kwa usafiri wa ndege, ikitokea jijini Dar es salaam, na jioni ilifanya mazoezi ya kujiweka sawa, kuelekea mchezo wake dhidi ya Biashara United Mara.
Wapinzani wao Biashara United waliwasili mjini humo Jana Jumatano (Juni 23) kwa usafiri wa basi dogo (Coaster), wakitokea moja kwa moja mjini Musoma, mkoani Mara.
Mchezo wa Nusu Fainali kati ya Miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara umepangwa kuanza majira ya saa tisa na nusu alasiri, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, Tabora.
Nusu Fainali nyingine ya Michuano hiyo itacheza mjini Songea mkoani Ruvuma, Uwanja wa Majimaji kati ya Mabingwa watetezi Simba SC dhidi ya Azam FC.