Mshambuliaji aliyezingiza klabu za Simba SC na Kagera Sugar katika mgogoro wa kimaslahi Yusuph Muhilu, amefunguka kwa mara ya kwanza, kufuatia sakata la uhamisho wake linaloendelea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Muhilu anadaiwa kusajiliwa na Simba SC kinyume na utaratibu, kufuatia Uongozi wa Kagera Sugar kuweka hadharani taarifa za kuwa na mkataba wa mwaka mmoja na mchezaji huyo, ambaye tayari ameshatambulishwa huko Msimbazi.
Mshambuliaji huyo amesema kulikua na mazingira ya kushawishiwa kusaini Simba SC kabla ya kuchukua maamuzi hayo, huku baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wakimthibitishia tayari wameshazungumza na Kagera Sugar.
Mbali na kuuzungumzia upande wa Simba SC, pia Muhilu amewaanika Viongozi wa Kagera Sugar kwa kusema walikua wanafahamu kilichokua kikiendelea, hadi alipofanya maamuzi ya kusajiliwa na Mabingwa hao wa Tanzania Bara.
“Nakumbuka Simba waliniambia kila kitu na Kagera wameshamalizana na nisaini mkataba wa miaka mitatu, hata nilipowafahamisha waajiri wangu (Kagera Sugar) wakati huo hawakupinga jambo hilo.”
“Hivyo mpaka nasaini na kutambulishwa niliamini tayari viongozi wa Simba na Kagera wamemalizana, lakini wakati huu ndio kuna jambo hilo linaendelea nadhani ni suala la kiutawala zaidi kuliko kwangu.”
Sakata la Muhulu kwa sasa linajadiliwa kibinafsi kati ya viongozi wa klabu ya Simba SC na Kagera Sugar, baada ya pande hizo mbili kukubaliana kulimaliza suala hilo nje ya Shirikisho la soka nchini TFF.