Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuchukua hatua kali kwa wasambazaji na wauzaji wa gesi za majumbani watakao pandisha bei za kesi bila kufuata sheria.

Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa ziara ya kushtukiza kwenye maduka mbalimbali ya wauza gesi na wasambazaji, huku akisistiza kuwa serikali haitokubali kuona wafanyabiashara wanajipangia bei kubwa ambazo zinawaumiza watanzania.

“Ninawapa onyo la mwisho wafanyabiashara wote wa gesi za majumbani kutopandisha bei, pia Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) walishatoa maelekezo, Mimi Waziri wa Nishati napita sasa kutoa onyo la mwisho, tukirejea wakati mwingine na kukuta bei imepanda tutachukua hatua ikiwa ni pamoja na kukufungia biashara husika kwa mtuhumiwa,” Amesema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani amefafanua kuwa, Mtungi wa ujazo wa kilo 6 unatakiwa kuuzwa kati ya shilingi 20, 000 hadi shilingi 21,000 na Mtungi wa ujazo wa kilo 15 unauzwa kati ya shilingi 47,000 hadi shilingi 50,000 na bei hiyo ni kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Amesema kuwa Serikali inafahamu bei ya gesi katika soko la dunia imepanda lakini si kwa kiasi kikubwa ambacho inawafanya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa hiyo hata kuliko namna ilivyopanda katika soko la dunia.

“Serikali inaendelea kufuatilia bei ya Soko la dunia na kama bei itapanda sana mtaelekezwa na kupewa utaratibu na EWURA lakini kwasasa haitapanda,” Amesema Waziri Kalemani.

Sambamba na hayo yote pia amewahasa wananchi kuwasilisha changamoto yoyote watakayoipata kwa Mamlaka ya Uthibti wa Huduma za Nishati na Maji EWURA ili waweze kupewa utaratibu unaotakiwa.

Yusuph Muhilu: Kagera Sugar walijua kila kitu
Kim Poulsen ataja kikosi Taifa Stars