Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa na sheria na miongozo 40 imeboreshwa sawa na majukumu ya baadhi ya taasisi yakilenga ili kuongeza ufanisi huku akiwataka wazalishaji Viwandani kuongeza thamani ya bidhaa ghafi zinazopatikana nchini.
Mpango ametoa wito huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya utoaji tuzo za Rais za wazalishaji bora Viwandani na kusema asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchi zinatumika katika kulipia uagizaji wa bidhaa ambazo nyingi zinaweza kuzalishwa nchini na kukidhi mahitaji ya ndani na kupunguza upotevu wa fedha za kigeni.
Amesema, “Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini ikiwemo kufanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti, na kuboreshwa kwa miundombinu ikiwemo nia ya kuiunganisha reli ya kisasa na nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutachochea biashara ya kikanda.”
Hata hivyo, amesema ili biashara iendelee kukua nchini, Serikali itaendelea kuboresha na kuongeza ufanisi wa bandari, kuboresha sekta ya nishati pamoja na miundombinu na kuliwezesha Taifa kunufaika na huduma na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi zitakazounganishwa na Reri hiyo ya Kisasa.