Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itahakikisha inatengeneza mfuko wa Hijja ili kuwapa fursa wale wote wasio na uwezo kwenda kufanya ibada ya hiyo.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ta Ikulu Zanzibar, Rais Mwinyi ameyasema hayo wakati akiwaaga Mahujaji watarajiwa wa Zanzibar, wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijja Makka, Saud Arabia mwaka huu.
“Mfuko wa Hijja utawasadia kwa kiasi kikubwa wale ambao hawana uwezo wa kwenda kutekeleza ibada hiyo huko Makka. sambamba na kufikia lengo na madhumuni ya kupata watu wengi kwenda Hijja,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewaomba waumini kuwa na subira kutokana na uwepo wa masharti ya umri katika ibada ya Hijja ya mwaka huu, huku akipongeza idadi ya Mahujaji waliojitokeza kwenda kutekeleza ibada hiyo licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza.
Kuhusu maombi ya Mahujaji kwa Serikali, Rais amesema Serikali itatizama uwezekano wa kuondosha cheti cha afya kama ilivyo kwa Tanzania Bara, na kusema amelipokea suala la akaunti maalum ya Zanzibar kwa ajili ya Hijja.
“Kuna kazi ya ziada ya kufanywa na Serikali, Taasisi pamoja na wananchi kwa ujumla ya kujifunza hasa kwa nchi zenye Waislamu wengi kama vile Malaysia na Indonesia ambapo huanza mipango ya kwenda Hijja mapema,” amefafanua Rais Mwinyi.
Awali Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amempongeza Rais Mwinyi kwa kufuatilia kwa karibu safari ya Hijja ya Mahujaji wa Zanzibar na kusisitiza kuiombea dua nchi iweze kuwa na maendeleo.
Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi amewaeleza Mahujaji hao umuhimu wa Hijja na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu huku Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Sheikh Abdalla Talib akisema alichokifanya Rais Mwinyi ni utamaduni wa muda mrefu uliowekwa.
Zanzibar, ilianza utaratibu wa kuratibu shughuli za Hijja toka mwaka 1923 ambapo kwa wakati huo ilikuwa ikiratibu kanda yote ya Afrika Mashariki, na mwaka 194 kundi la kwanza kusafiri kwa ukanda wa Afrika Mashariki lilitokea mjini Zanzibar.