MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Zanzibar Othman Masoud Othman, amesema chama hicho kinafanya kazi kubwa ili Zanzibar iwe na mazingira bora ya uchaguzi Zanzibar iwe na mazingira bora ya uchaguzi wa kidemokrasia na kuwezesha kuzuia matatizo ya uvunjivu wa amani wakati wa uchaguzi.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo Wilaya ya Kati Unguja, wakati akizungumza baada ya kufungua Ofisi za chama hicho Jimbo la Tunguu Mkoa wa Kati Kichama.
Amesema, kwa kuzingatia uzalendo na nia na njema ya Kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, chama hicho kupitia viongozi wake kimekuwa kikishiriki vyema kutoa mapendekezo kuhusu uundwaji wa Katiba mpya ya Tanzania na kwamba kimewasilisha maoni yake kwa maandishi juu ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika suala hilo.
“Suala hili limekuwa likifanywa kwa kuzingatia uzalendo mkubwa unaofanywa na viongozi wa ngazi tofauti kwa nia ya kuhakikisha kwamba taifa linajenga mazingira bora ya uchaguzi wa kidemokrasia na Amani ya kweli,” amesema Mkamu Othman.
Kuhusu suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Othman amesema Viongozi waliomo serikali waendelea kujitahidi katika kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wa majukumu ya waliopewa, kwa kuwa wamekula kiapo cha kuwatumika wananchi kwa uadilifu na utiifu mkubwa.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi katika kujenga nchi kwa kuunga mkono jitihada za viongozi mbali mbali katika kuhakikisha wanatimiza vyema wajibu waliopewa wa kuitumika ipasavyo nchi yao.
Kuhusu Kauli za ukosoaji kwa viongozi zinazotolewa na chama hicho, Othman amesema, “kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wa kuisaidia nchi ili iweze kuwatumikia vyema wananchi kwa uzalendo na taifa liweze kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi zaidi.”
Aidha, akizungumzia suala la Sensa ya Watu na Makaazi , Othman amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa jumla kuhakikisha kwamba wote wanashiriki kuhesabiwa kwa kutoa mashirikiano ipasavyo siku itakapowadia.
“Sensa ni jambo muhimu litakalowezesha taifa kupata takwimu na tarifa sahihi za aina mbali mbali na kusaidia serikali kuweza kupanga mipango mbali mbali ya maendeleo kwa kutumia matokeo ya taarifa zitakazopatikana kwenye sensa,” amesema.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Nassor Ahemed Mazrui ambaye pia ni waziri wa Afya Zanzibar, amesema viongozi wa chama hicho wataendelea kutekeleza majukumu ya kiserikali waliyopewa kwa uzalendo mkubwa ili kusaidia jitihada za unjenzi wa nchi kupitia serikali ya Umoja wa Kitaifa ilipo.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban, amesema kwamba pamoja na majukumu ya kiserikali waliyopowa pia viongozi wa Chama hicho wataendelea na jitihada za kukiimarisha chama hicho kwa ujenzi wa ofisi na kuimarisha wanachama katika majimbo mbali mbali nchini.