Wachezaji Yahya Zaydi na Ally Niyonzima hawatokuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC, kitakachoikabili Simba SC, keshokutwa Jumamosi (Juni 26), kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Tayari Azam FC imeshawasili mjini Songea na kuanza maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka mkoani Ruvuma na mikoa ya karibu.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema watawakosa wachezaji wawili ambao ni Yahya Zaydi na Ally Niyonzima wanaosumbuliwa na majeraha.
“Yahya Zaydi na Ally Niyonzima wamebaki Dar es salaam, wakiendelewa na matibabu, hivyo hatutakuwa nao kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba SC keshokutwa Jumamosi.”
“Tumejiandaa vizuri na benchi la ufundi linaendelea kufanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo, ambao tunaamini wachezaji wetu watapambana na kupata matokeo yatakayotupeleka fainali ya ASFC.” Amesema Zaka Zakazi.
Azam FC iliwasili mjini Songea mkoani Ruvuma jana Jumatano (Juni 23), ikitokea Dar es salaam kwa usafiri ndege, sawa na Simba SC ambayo ilitangulia kufika mjini humo na kupokelewa kwa shangwe na wanachama pamoja na mashabiki wao.