Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amewasili jijini Paris nchini Ufaransa leo Jumamosi Novemba 14, akianza ziara yake ya siku saba barani Ulaya na Mashariki ya kati.
Ziara ya hii ya Pompeo yenye lengo la kuimarisha na kuunga mkono vipaumbele vya Rais anayeondoka madarakani Donald Trump, inachukuliwa kama kitu kisichokuwa cha kawaida kutokana na kuwa takriban nchi zote alizopangiwa kuzitembelea zimeshampongeza Joe Biden kwa ushindi wake katika kiti cha Urais wa Marekani.
Pompeo anatarajiwa pia kwenda Mashariki ya kati, atakakotembelea makazi ya Israel ya walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, makazi ambayo mawaziri wengine wa mambo ya nje wa Marekani waliomtangulia walijiepusha kuyatembelea.
Ikumbukwe kwamba hadi sasa mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani pamoja na rais wake na wanachama wengine wengi wa chama cha Republican hawajakubaliana na matokeo ya uchaguzi wa Marekani.