Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira, January Makamba amesema kuwa Ziwa Jipe liko hatarini kutoweka endapo hatua za haraka hazitachukuliwa katika kulinusuru ziwa hilo.
Waziri Makamba amesema hayo leo Machi 26, 2017 wakati akifanya ziara ya kukagua ziwa hilo lililopo katika Kata ya Jipe Wilayani Mwanga, Kilimajaro ambalo sehemu kubwa imezungukwa na magugu maji.
Waziri Makamba kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamiza wa Mazingira (NEMC) ameazimia kutangaza kupita Tangazo la Serikali kuwa eneo hilo ni eneo nyeti kimazingira, hivyo amesema kuwa ni lazima kuwe na mpango wa muda mfupi na ule wa muda mrefu wa kulinusuru.
”Tutatanga eneo hili kuwa eneo nyeti kimazingira na tutaweka masharti ya matumizi katika eneo hili” Amesisitiza Makamba
Amesema kuwa eneo la ziwa hilo pia litawekwa chini ya uangalizi maalumu na kuweka masharti ya matumizi bora ya eneo hilo. ” Tutaweka masharti makali na magumu zaidi ili watakao kiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria”.
“Bila hifadhi ya mazingira hakuna maisha, na ukiyaharibu mazingira hakuna msamaha yatakuadhibu tu” amesema Waziri Makamba.
Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa shughuli zozote za maendeleo iwe uvuvi, kilimo, utalii, mifugo kwa namna moja ama nyingine zinategema hifadhi endelevu ya mazingira, hivyo amewataka wasimamizi wa Bonde la Pangani, Wizaya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukutana mara moja kuandaa mpango na mtazamo wa pamoja wa kunusuru Ziwa Jipe.
Pia, Waziri Makamba amefanya ziara katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji cha Kakongo ambao kwa pamoja wamelalamikia zuio la kufanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo kutokana na kupungua kwa kina cha maji na samaki katika bwawa hilo.
Kufuatia malalamiko hayo ya Wananchi, Waziri Makamba ameagizia kufanyika kwa doria na kuainisha pampu zote zinazovuta maji kutoka bwawani hapo.
“Naaagiza Mamlaka ya Wilaya ya Mwanga, Serikali ya Mtaa na Mamlaka ya Bonde Pangani kufanya doria na kuhakiki pampu zote kujua uhalali wake kama zimesajiliwa na kama zinavibali, zitakazobainika kutokuwa na vibali zote zitaifishwe” Amesema Waziri Makamba.