Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema zoezi la chanjo ya Uviko-19 limefikia zaidi ya asilimia 80 na chanjo zilizobakia mikoani hivi sasa ni chache.
Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 4 2021, wakati akifungua kongamano la tano la uwezeshaji lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Neec).
Kauli hiyo imekuja baada ya Serikali kuanzisha kampeni maalum ya kuhamasisha uchanjaji wa chanjo hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo makanisani na kwenye mikusanyiko ya watu huku kukiwa na huduma ya chanjo inayotembea.
“Tunalo zoezi la uchanjaji. Namshukuru Mungu tumefikia asilimia 80 na kitu huko, tumebaki na chanjo chache sana kwenye mikoa hiyo, kila mmoja awahi huko na kama kuna mahitaji tutaleta nyingine malengo ni afya,”amesema Majaliwa.
Jumla ya chanjo milioni 1.058 zilipokelewa nchini kutoka nchini Marekani Julai 24, 2021 na uchanjaji ulizinduliwa rasmi Julai 29, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan.