Maafisa wa serikali nchini Kenya, wamesitisha zoezi la kutafuta miili ya watu waliopoteza maisha na kuzikwa katika kijiji cha Shakahola karibu na mji wa Malindi Pwani baada ya mhubiri Paul Mackenzie Nthenge, kuwaambia wasile chakula mpaka wafe ili wakakutane na Mungu.
Waziri wa usalama wa ndani, Kithure Kindiki amesema mpaka sasa miili 90 imefukuliwa, idadi kubwa ikiwa ni ya watoto na wanawake wakati huu zoezi hilo likisitishwa kwa muda kutokana na kukosekana kwa sehemu ya kuhifadhi miili zaidi.
Amesema, Mchungaji Mackenzie anastahili kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC kwa ugaidi kwa mauaji ya halaiki, kufuatia mafundisho yake yenye utata yaliyosababisha wafuasi wake hao kufunga hadi kifo na kusema watu wana uhuru wa kuabudu lakini wasitimie hali hiyo kuwaumiza.
Mapema wiki hii Rais wa Kenya, William Ruto, naye alimfananisha Mchungaji huyo na gaidi na kuahidi kuchukua hatua kali kwa wahubiri kama hao, huku tukio hilo limewashangaza Wakenya na kuacha maswali ya kwanini imechukua muda mrefu kubaini tukio hilo.