Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki amesema ziara ya Michezo ya Kimataifa ya Kirafiki nchini Sudan, imekisaidia kikosi chake kuendelea kuimarika, katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa msimu 2022/23.
Simba SC ilialikwa Sudan kushiriki Michuano maalum iliyoandaliwa na Klabu ya Al Hilal katika mji wa Khartoum, ambapo imecheza michezo miwili dhidi ya Asante Kotoko (Ghana) na Wenyeji.
Kocha Zoran Maki amesema michezo hiyo imekisaidia sana kikosi chake kuwa katika hali nzuri ya kiushindani, huku akijipanga kupambana katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC na ule wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Malawi Nyasa Big Bullet.
“Michezo tuliocheza hapa Sudan imezidi kutuimarisha na kutujenga zaidi, nimekuwa na kipindi kizuri kuimarisha kikosi chetu hivyo naamini mchezo ujao dhidi ya KMC FC na ule ya Ligi ya Mabingwa tutafanya vizuri.” amesema Kocha Zoran
Kwenye Michuano ya Kimataifa ya Kirafiki, Simba SC iliifunga Asante Kotoko ya Ghana 4-2 kabla ya kupoteza kwa 1-0 dhidi ya wenyeji Al Hilal jana Jumatano (Agosti 31).
Simba SC inatarajia kurejea jijini Dar es salaam leo Alhamis (Septemba Mosi) ikitokea Sudan, huku Jumamosi (Septemba 03) ikitarajia kucheza mchezo mwingine wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Arta Solar ya Djibout.