Kocha wa Viungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Adel Zrane amemaliza utata wa Mustakabali wa Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere kwa kusema, bado anahitajika klabuni hapo.
Kagere amekua akihusishwa na mpango wa kuachwa mwishoni mwa msimu huu, na nafasi yake huenda ikajazwa na mshambuliaji mwingine wa kimataifa, hali ambayo ilizua maswali mengi miongoni mwa mashabiki na wanachama wa Simba SC.
Kocha Zrane amesema Mshambuliaji huyo bado ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri ndani ya kikosi cha Simba, tofauti na misimu miwili iliyopita, hivyo hatarajiwi kuachwa ama kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Kagere msimu huu amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, kutokana na ushindani mkubwa wa namba anaoupata kutoka kwa washambuliaji Chris Mugalu na John Bocco.
Hata hivyo mara kadhaa Mshambulaiji huyo aliyeibuka kidedea kwenye orodha ya wapachika mabao kwa msimu miwili mfululizo, amewahi kusema bado anataka kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza, na hatamani kuondoka Simba SC.
Kwa msimu huu Kagere ameshaifungia Simba mabao 11 kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akitarajiwa kuendelea kufunga endapo atapewa nafasi na kocha Didier Gomes katika michezo iliyosalia.