Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewahakikishia wafugaji wa samaki nchini kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wafugaji kufuga samaki.
Ulega amebainisha hayo kwenye mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa wa Shinyanga uliofanyika katika ukumbi wa NSSF mjini Shinyanga jana, ambapo mgeni rasmi alikuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya uwekezaji, Angellah Kairuki.
Ulega amesema mabwawa ya samaki yameongezeka kutokana na jitihada zilizopo na kueleza namna serikali inavyoendelea kudhibiti uvuvi haramu Baharini na kwenye Maziwa.
“Kabla ya serikali ya awamu ya tano katika Ziwa Victoria tulikuwa na vizimba vya ufugaji wa samaki visivyozidi 50 hivi leo tuna vizimba zaidi ya 400 vya ufugaji wa samaki maana yake mwitikio ni mkubwa sana baada ya kufanyika jitihada za makusudi kwamba haturuhusu samaki kuingia Tanzania kwa sababu sisi tuna uwezo wa kufuga na wenyewe kuweza kutumia.” Ameeleza Ulenga