Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, leo Mei 26, amesimama kizimbani na kukana mashtaka 18 yanayomkabili .
Katika kesi ya msingi iliyosikilizwa mahakamani jijini Pietermaritzburg, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa Rais kati ya mwaka 2009 na 2018 anakabiliwa na tuhuma za rushwa, ukwepaji kodi na utakatishaji fedha.
Zuma, anayekabiliwa na uchunguzi mwingine wa ufisadi uliofanywa wakati akiwa rais, anatuhumiwa kwa kukubali dola 34,000 kila mwaka kutoka kwa kampuni ya silaha ya Ufaransa, Thales, ili nayo kampuni hiyo ilindwe dhidi ya uchunguzi kuhusiana na biashara hiyo.
Akizungumza kwa upole, huku watu wanaomuunga mkono wakiwa wamekusanyika nje ya mahakama, Zuma mwenye umri wa miaka 79 amesema kesi zake ni matokeo ya siasa chafu dhidi yake.
Akifafanua hilo, Zuma hakuwataja majina lakini alisema maadui zake wanatoka ndani na nje ya Chama tawala, African National Congress (ANC).
Mawakili wa Zuma wanataka mwendesha mashitaka wa serikali Billy Downer aondolewe kwenye kesi hiyo, kwa misingi kuwa hana mamlaka ya kuongoza kesi hiyo.
Upande wa mashitaka umeomba muda zaidi kujibu ombi hilo na uamuzi utafanywa Julai 19.