Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Viongozi mbalimbali nchini kuzungumza na wananchi suala la ukomeshaji wa unyanyasaji wa kijinsia ili kujenga jamii iliyo bora na inayojiamini.

Dkt. Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, amesema hayo wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Bulega wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni siku ya Pili ya ziara yake katika Jimbo hilo.

Amesema, “Viongozi wakati mnazungumza na wananchi kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo mkumbuke kueleza suala la ukomeshaji wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia ili watu wajue kuwa vitendo hivi vinakera Taifa na hivyo sisi tunawajibu wa kulikemea suala suala hili.”

Dkt. Biteko amesema kuwa, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ukatili wa wanawake na watoto pamoja na ubakaji vinakera, hivyo Taifa linapaswa kuvikemea na kumtaka kila mwananchi kuwa makini na malezi ya watoto ili kutowaweka katika mazingira hatarishi.

Akizungumzia maendeleo ya Jimbo la Bukombe, Dkt.Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya barabara, afya shule na kueleza kuwa nia ya Rais ni kupelekea maendeleo watu wake hivyo amewaomba wananchi kumuombea na kuendelea kumuunga mkono.

Aidha amewapongeza madiwani wote katika Jimbo la Bukombe kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kusimamia miradi kwenye Sekta za elimu, afya, barabara na kwamba anaona fahari kuwa na madiwani hao pamoja na wananchi ambao wameonesha kuwa na uchungu na maendeleo.

Vijana sita wazishitaki nchi 32 kwa kutochukua hatua
Majaribio uendeshaji SGR kuanza Desemba