Balozi wa Uingereza nchini Marekani, Kim Darroch ametangaza kujiuzulu mara baada ya kuvuja kwa barua pepe zilizokuwa zikiukosoa utawala wa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Amesema kuwa ni vigumu kwake kuendelea kutumikia katika wadhifa wake wa ubalozi kufuatia kuvuja kwa taarifa za kidiplomasia zilizokuwa na ukosoaji wake dhidi ya rais wa Marekani.

Katika barua ya kujiuzuli kwake, Darroch amesema kuwa ingawa wadhifa wake huo ulikuwa umalizike mwisho wa mwaka 2019, anaamini hali ilivyo kwassa ni bora kuwajibika ili uteuzi wa balozi mwingine ufanyike.

Darroch katika kumkosoa Trump ilikuwa pamoja na kumuelezea kiongozi huyo wa Marekani kama ni mtu asiyejiweza, asiyejiamini, asiyekuwa na uwezo wa uongozi katika serikali yake.

Aidha, taarifa hizo zilizovujishwa zilikuwa zinapelekwa kwa maafisa wa ngazi ya juu wa Uingereza, ambapo wachunguzi wanaamini kuwa aliyevujisha habari hizo atapatikana na atakuwa ni kati ya wanasiasa wa Uingereza na siyo serikali ya kigeni.

Akizungumza katika Bunge la Uingereza, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amethibitisha kujiuzulu kwa Kim Darroch.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani alijibu mara baada ya kuvuja kwa nyaraka hizo za siri kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa kijamii, kwa kumuita Darroch ‘mtu mpuuzi sana na mpumbavu mwenye kiburi na hatafanya naye tena kazi’

Video: Aliyetaka kumtapeli DC Joketi anaswa na Takukuru
Serikali yawashika mkono wabunifu, yatoa milioni 700