Aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha The Playlist cha Times FM, Omary Tambwe maarufu kama Lil Ommy amehamia rasmi Wasafi FM na kutambulisha kipindi kipya ‘The Switch’.

Lil Ommy ambaye ni Mtangazaji Bora Afrika (2019) kwa mujibu wa Tuzo za African Entertainment Awards – USA (AEAUSA) zilizotolea jijini New York nchini Marekani, juzi, Machi 31, 2020 alianza rasmi kusikika hewani kupitia kituo hicho akiitambulisha ‘The Switch’ inayoruka kuanzia saa 8 mchana hadi 11 jioni siku za kazi.

Mtangazaji huyo anayefahamika pia kama ‘Mfalme wa Mahojiano (King of Interviews), hivi sasa ni mwanafamilia wa kikosi kazi cha burudani kinachoiwasha ‘The Switch’ kilichobatizwa ‘mafundi wa burudani’. Kikosi hicho pia kinaundwa na Ammy Girl, Raymond Mshana, DJ Vasley na mtayarishaji ni Allen Donald.

Ikiwa ni siku ya kwanza kusikika, kipindi hicho kilipokewa vizuri na wasikilizaji kikiwa kinaruka mubashara kupitia YouTube Channel, ambapo mrejesho wa jumbe za wasikilizaji/watazamaji ulitoa picha ya mapokeo makubwa.

Ubunifu ulitawala kuitambulisha ‘The Switch’, ambapo ‘mafundi wa burudani’ waliingia wakiwa wamevalia mavazi ya ufundi waya mithili ya mafundi wa Shirika la Umeme, wakiwa kwenye gari lenye mfanano huo pia. Kwa namna yake waliingia studio iliyoko ghorofani kwa kutumia ngazi wakipita dirishani. Kisha, wakaiwasha rasmi ‘The Switch’!

Diamond Platinumz ambaye pia ni mmiliki wa kituo hicho, alifunguka kupitia Instagram, akieleza nia ya kuendelea kukipeleka kiwanda cha burudani kwenye hatua nyingine kupitia ‘The Switch’.

“Let’s continue taking our Entertainment industry to the Next Level,” aliandika Diamond kwenye tangazo la kutambulisha kipindi hicho lililowekwa na Lil Ommy kwenye Instagram.

Watu wengi maarufu waliofuatilia uzinduzi wa kipindi hicho walieleza jinsi walieleza jinsi walivyovutiwa na kipindi hicho. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, Lavalava, Diamond Platinumz ni miongoni mwa wengi walionesha mtandaoni kupenda walichosikia kuhusu ‘The Switch’.

Mtwara ruksa kunywa gongo ya mabibo
LIVE: Kinachojiri mazishi ya mwanahabari TBC, Marin Hassan Marin