Michezo ya kubahatisha maarufu kama beti (betting) iliyoshamiri hivi sasa nchini ikiahidi kutoa mamilioni kwa washindi iko hatarini kuyeyuka, baada ya Rais John Magufuli kuonesha kukubaliana na ushauri aliopewa na viongozi wa dini jana jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wa dini walieleza kuwa mchezo huo wa ‘kubeti’ ni kamari ambayo vitabu vitakatifu vinapiga marufuku, lakini pia ni chanzo kikuu cha kupoteza nguvu kazi hasa kwa vijana ambao baadhi yao wamedaiwa kupata ulaibu wa mchezo hiyo na kuacha kufanya kazi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora Tanzania, Zainuddin Adamjee, alisema kuwa wapo vijana ambao tuhumia zaidi ya shilingi 10,000 kila siku kucheza kamari wakiamini kuwa watapata mamilioni, hivyo alimuomba Rais Magufuli kulitazama na ikiwezekana kuzuia michezo hiyo.

“Mheshimiwa Rais, hata katika Quran na Biblia tumeambiwa kamari ni haramu,” aisema Adamjee na kuongeza, “tunasema awamu hii ni ‘hapa kazi tu’, lakini kwao ni ‘hapa kamari tu’.”

Rais Magufuli alijibu maombi ya kiongozi huyo wa dini akimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulifanyia kazi.

“Hili la kamari, Mzee Adamjee nimelisikia na Waziri Mkuu amelisikia. Kwa sababu nchi nyingine haya mambo ya kamari hata hayatangazwi. Lakini siku hizi watu wameshajenga spirit (ari) hata watoto, kwamba ukicheza hiki utapata tu,” alisema Rais Magufuli.

“Hii inajenga element ya uvivu na element ya kutokufanya kazi. Hata kama Serikali inakusanya mapato… na kwenye vitabu vya Mungu, Quran au Biblia kamari ni mbaya,” aliongeza akifafanua kwa mfano wa Yesu Kristo kupindua meza za wafanyabiashara na wacheza kamari aliowakuta wakifanya shughuli hizo kwenye nyumba ya ibada.

Mbali na suala hiyo la kamari, katika kikao hicho, Rais Magufuli alijibu maombi mengi yaliyowasilishwa na viongozi hao wa dini yaliyogusia masuala ya demokrasia, huduma ya maji, kutengwa kwa maeneo ya kuabudia makazini na katika maeneo ya viwanja vya ndege kwa dini zote, mavazi yenye kuzingatia maadili, elimu ya dini, kilimo na uwekezaji.

Video: NEMC yawageukia wamiliki wa migodi, sasa kukumbana na adhabu kali
Video: Chalamila ahoji uwepo wa madini, 'Yako wapi madini Mbeya?

Comments

comments