Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rose Mdenye ( 31) ameuawa kwa shambulio la kuchomwa kisu linalosadikika kufanywa na mume wake kwa kile kinachodaiwa ni sababu za  wivu wa mapenzi.

Marehemu ameacha mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na mwili wake kuugwa leo na kusafirishwa wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa mazishi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Caroline Damiani amesema walimpokea marehemu huyo jana saa 5.30 usiku akiwa tayari ameshafariki dunia huku akiwa na majeraha makubwa katika mwili wake akitokea katika eneo la Swaswa umbali wa kilometa 15 toka Jijini Dodoma.

Naye Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Beatrice Mtenga amesema walipata taarifa za mhadhiri huyo kuchomwa kisu na mume wake jana usiku na kudai kuwa walikuwa hawamfahanu mume wa mhadhiri Mdenye lakini wanaendelea kutafuta habari zake na watatoa taarifa zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Jiji la Dodoma, Gilles Muroto amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akidai kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi  kuhusu chanzo cha kifo hiko ili hatua kamili zichukuliwe.

Mdenye alikuwa mhadhiri wa kompyuta baada ya kusoma shahada ya kompyuta Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kati ya 2007-2010 na akasoma shahada ya uzamili Udom kati ya 2013-15.

Aidha wanachuo zaidi ya 3,000-5000 aliowahi kuwafundisha wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mhadhiri wao marehemu Rose Mdenye.

Mungu aipumzishe roho ya marehemu Mdenye mahali pema peponi.

 

Marais wa Korea Kaskazini na kusini wakutana kwa dharula
Waziri afanya ziara ya kushtukiza Uwanja wa ndege