Kufuatia kifo cha Mbunge wa Korogwe vijijini (CCM), Steven Ngonyani maarufu kama Prof. Maji Marefu kilichotokea usiku wa kuamkia leo kimeweza kumuibua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba na kuungana na viongozi wengine wa CCM katika kutoa salamu za pole.

Dkt. Nchemba ambaye amevuliwa wadhifa wake wa Uwaziri wa Mambo ya Ndani na Rais Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita, kupitia mtandao wake wa kijamii amesema kuwa CCM imepata pigo kubwa kwa kumpoteza kada na kiongozi wa kweli.

“Maandiko matakatifu yanasema, mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi. tumempoteza kaka, ndugu na rafiki comrade Steven Hilary Ngonyani (Prof. Maji Marefu), tumempoteza kiongozi na kada kweli kweli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),”ameandika Mwigulu.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa pole zake kwa familia huku akiwataka wawe na ustamilivu katika kipindi hiki kigumu walichokuwa nacho.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameguswa na kifo hicho cha kada wa CCM na kumuombea dua marehemu huko aendapo.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa Korogwe vijijini, Steven Ngonyani amefariki akiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ambayo yaliyokuwa yanamsibu na kufanya idadi ya Wabunge waliofariki kufikia watano hadi hivi sasa wakiwemo wanne wa majimbo na mmoja wa viti maalumu.

Utaratibu wa kuaga mwili wa Prof. Maji Marefu wapangwa
Daktari bingwa afunguka kuhusu magonjwa ya Moyo

Comments

comments